Page 150 - Your Guide to University Life
P. 150
Kujiandaa na maisha ya mtaani toka ukiwa chuo
Kitu kimoja ambacho natamani ningekifanya au ningeanza kukifikiria mapema toka nikiwa chuo ni maisha baada ya chuo, kujiandaa na maisha hayo toka nikiwa chuo ili nikimaliza nisipate hata sonona maana msongo wa mawazo huwaga mkubwa na kukosa maandalizi ya njia gani utatembea mtaani kunazidishaga sonona kwa wahitimu.
Ukweli ni kuwa soko la ajira lina mashindano sana, nakumbuka nilipokuwa namaliza chuo hata sikulijua hili nilijua tu nitatuma maombi nitaitwa na kutakuwa hakuna watu wengi, nitafanya usaili wataniambia njoo uanze kazi Jumatatu.
Mtaani nikakutana na mambo tofauti kabisa, mkiitwa usaili, unakuta mpo wengi kiasi kwamba haujui mwisho wa mstari, kazi inayohitaji watu nane, waejitokea hata 2000+, na ukiachana na hilo ambalo linaongeza ushindani wa ajira, kuna pia wale matapeli wanaotumia shida za watafuta ajira kuwaibia, kuwaomba rushwa za pesa au ngono na kuwapotezea muda nk.
Nahisi pia jambo lingine ambalo linaendana na hili ni kupunguza matarajio, matarajio yangu yalikuwa makubwa sana nilipokuwa namaliza chuo kiasi kwamba nilipokutana na hali ya tofauti mtaani nilivunjika moyo, nilipoteza kidogo mwelekeo wa kujua naanzaje lakini pia nilipata sonona, woga na kutokujua huko mbele maisha yangu yatakuwaje. Ndio maana kila nikiangalia nyuma natamani niwe nilishaanzaga kufikiria kuhusu maisha ya mtaani toka nilipokuwa chuo.
150